Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 5

5
Maombolezo na wito wa toba
1Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:
2“Bikira Israeli ameanguka,
kamwe hatainuka tena,
ameachwa pweke katika nchi yake,
hakuna yeyote wa kumwinua.”
3Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,
mia moja tu watarudi;
wakati mji utakapopeleka mia moja,
kumi tu ndio watarudi hai.”
4Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli:
“Nitafuteni mpate kuishi;
5msitafute Betheli,
msiende Gilgali,
msisafiri kwenda Beer-Sheba.
Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni,
na Betheli itafanywa kuwa ubatili#5:5 yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni (taz. Hosea 4:15)..”
6Mtafuteni Mwenyezi Mungu mpate kuishi,
au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto;
utawateketeza, nayo Betheli
haitakuwa na yeyote wa kuuzima.
7Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu
na kuiangusha haki chini
8(yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko
na mchana kuwa usiku,
ambaye huyaita maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya nchi:
Mwenyezi Mungu ndilo jina lake;
9yeye hufanya maangamizi kwenye ngome
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
10mnamchukia yule akemeaye mahakamani,
na kumdharau yule ambaye husema kweli.
11Mnamgandamiza maskini
na kumlazimisha awape nafaka.
Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,
hamtaishi ndani yake;
ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,
hamtakunywa divai yake.
12Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu
na ukubwa wa dhambi zenu.
Mmewadhulumu wenye haki na kupokea rushwa
na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
13Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza nyakati kama hizo,
kwa kuwa nyakati ni mbaya.
14Tafuteni mema, wala si mabaya,
ili mpate kuishi.
Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni
atakuwa pamoja nanyi,
kama msemavyo yupo nanyi.
15Yachukieni maovu, yapendeni mema;
dumisheni haki mahakamani.
Yamkini Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
atawahurumia mabaki ya Yusufu.
16Kwa hiyo hili ndilo Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo:
“Kutakuwa na maombolezo barabarani zote,
na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.
Wakulima wataitwa kuja kulia,
na waombolezaji waje kuomboleza.
17Kutakuwa na kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,
kwa kuwa nitapita kati yenu,”
asema Mwenyezi Mungu.
Siku ya Mwenyezi Mungu
18Ole wenu ninyi mnaoitamani
siku ya Mwenyezi Mungu!
Kwa nini mnaitamani siku ya Mwenyezi Mungu?
Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
19Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba
kumbe akakutana na dubu,
kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake
na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,
kumbe akaumwa na nyoka.
20Je, siku ya Mwenyezi Mungu haitakuwa giza, na si nuru:
giza nene, bila mwali wowote?
21“Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
22Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,
sitazikubali.
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,
sitazitambua.
23Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
24Lakini acheni haki itiririke kama mto,
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
25“Je, mliniletea dhabihu na sadaka
kwa miaka arobaini kule jangwani,
ee nyumba ya Israeli?
26Mmeyainua madhabahu ya Sikuthi
mungu wenu mtawala,
na Kiuni mungu wenu wa nyota,
ambao mliwatengeneza wenyewe.
27Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”
asema Mwenyezi Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi ya mbinguni.

Iliyochaguliwa sasa

Amosi 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia