Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 9

9
Kuokoka kwa Sauli
(Matendo 22:6-16; 26:12-18)
1Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana Isa, akamwendea kuhani mkuu, 2naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mfuasi yeyote wa Njia Ile#9:2 Njia Ile maana yake wafuasi wa Isa (Yohana 14:6; Matendo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi., akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. 3Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza pande zote. 4Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”
5Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”
Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Isa unayemtesa. 6Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa unachopaswa kufanya.”
7Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza hadi Dameski. 9Kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu; naye hakula wala kunywa chochote.
10Huko Dameski kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana Isa alimwita katika maono, “Anania!”
Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”
11Bwana Isa akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
13Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. 14Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”
15Lakini Bwana Isa akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo nilichochagua kutangaza jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na watu wa Israeli. 16Nami nitamwonesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”
17Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Isa aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu wa Mungu.” 18Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa. 19Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.
Sauli ahubiri Dameski
20Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba Isa Al-Masihi ni Mwana wa Mungu#9:20 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.. 21Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” 22Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Isa ndiye Al-Masihi#9:22 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..
23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakapanga njama kumuua Sauli. 24Lakini Sauli akagundua njama yao. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua. 25Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.
Sauli huko Yerusalemu
26Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. 27Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana Isa, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Isa huko Dameski. 28Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana Isa. 29Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani, lakini wao walijaribu kumuua. 30Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.
31Ndipo waumini katika Yudea yote, Galilaya na Samaria wakawa na wakati wa amani. Likatiwa nguvu; na kwa kuwezeshwa na Roho wa Mungu, idadi yao ikaongezeka, na wakaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
Matendo ya Petro
(Matendo 9:32–12:25)
Kuponywa kwa Ainea
32Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alienda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida. 33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, aliyekuwa amepooza na kwa muda wa miaka nane alikuwa hajatoka kitandani. 34Petro akamwambia, “Ainea, Isa Al-Masihi anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. 35Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana Isa.
Petro amfufua Dorkasi
36Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi#9:36 Tabitha kwa Kiaramu na Dorkasi kwa Kiyunani yote yamaanisha Paa.). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37Wakati huo akaugua, akafa, na wakauosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”
39Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao. Alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.
40Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana Isa. 43Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia