Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 18

18
Paulo huko Korintho
1Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho. 2Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mzawa wa Ponto, aliyekuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona, 3naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao. 4Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi#18:4 Nyumba ya ibada na mafunzo., akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
5Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Isa ndiye Al-Masihi#18:5 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.. 6Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakung’uta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”
7Kisha akaondoka kwenye sinagogi, akaenda nyumbani mwa Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu; nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi. 8Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.
9Usiku mmoja Bwana Isa akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze, 10kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa nina watu wengi katika mji huu.” 11Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha Maandiko ya Mungu.
12Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani. 13Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”
14Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza. 15Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.” 16Akawafukuza kutoka mahakamani. 17Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.
Paulo arudi Antiokia
18Baada ya kukaa Korintho kwa muda, Paulo akaagana na ndugu, akasafiri kwa meli kwenda Siria akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea, Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri. 19Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi. 20Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali. 21Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa meli kutoka Efeso. 22Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kuwasalimu waumini, kisha akaenda Antiokia.
Safari ya tatu ya Paulo kueneza Injili
(Matendo 18:23–21:16)
23Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.
Huduma ya Apolo huko Efeso na Korintho
24Basi akaja Efeso Myahudi aliyeitwa Apolo, mzawa wa Iskanderia. Alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa na ujuzi wa Maandiko. 25Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana Isa, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi kuhusu Isa, ingawa alijua tu ubatizo wa Yahya. 26Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimwalika kwao na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.
27Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. 28Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akithibitisha kwa Maandiko kwamba Isa ndiye Al-Masihi.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 18: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia