Matendo 17
17
Ghasia huko Thesalonike
1Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2Kama ilivyokuwa desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwa Maandiko, 3akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Al-Masihi#17:3 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Isa ninayewaambia habari zake, ndiye Al-Masihi.” 4Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.
5Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani mwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye umati ule wa watu. 6Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipaza sauti na kusema: “Watu hawa walioupindua ulimwengu wamekuja huku, 7naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Isa.” 8Waliposikia haya, umati ule wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia. 9Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaachia waende zao.
Paulo na Sila huko Beroya
10Usiku ule ule, wale ndugu wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi. 11Hawa Waberoya walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli. 12Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume Wayunani wa tabaka la juu.
13Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea. 14Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya. 15Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye hadi Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.
Paulo huko Athene
16Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu. 17Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko. 18Kundi la wenye falsafa, Waepikureo#17:18 Waepikureo waliamini kwamba anasa aina mbalimbali, hasa za mawazo, ndizo lengo la maisha. na Wastoiko#17:18 Wastoiko waliamini kwamba maisha hayapaswi kuwa ya hisia ya furaha wala huzuni kupita kiasi., wakajibizana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri Injili kuhusu Isa na ufufuo wa wafu. 19Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago#17:19 maana yake baraza la viongozi au wanafalsafa wa mji wa Athene; walikutana katika kilima cha Aresi, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini? 20Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.” 21(Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya.)
22Ndipo Paulo akasimama katikati ya mkutano wa Areopago, akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. 23Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa makini vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa:
Kwa Mungu Asiyejulikana.
Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.
24“Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo, ndiye Bwana wa mbingu na nchi; hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28‘Kwa kuwa ndani yake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni uzao wake.’
29“Kwa kuwa sisi ni uzao wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Al-Masihi kutoka kwa wafu.”
32Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.” 33Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao. 34Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao walikuwemo Dionisio, mmoja wa mkutano wa Areopago, na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari, na wengine wengi.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.