Matendo 16:22-34
Matendo 16:22-34 NENO
Umati wa watu wakajiunga kuwashambulia Paulo na Sila, na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wapigwe mijeledi. Baada ya kuwapiga sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo. Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. Lakini Paulo akapaza sauti kwa nguvu, akisema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!” Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?” Wakamjibu, “Mwamini Bwana Isa Al-Masihi, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” Wakamwambia neno la Bwana Isa, yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake. Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.