Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 16:22-34

Matendo 16:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Kundi la watu likajiunga likawashambulia; na wale mahakimu wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakaamuru wapigwe viboko. Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali. Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo. Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana. Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua. Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.” Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu. Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?” Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.” Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake. Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. [ Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu].

Shirikisha
Soma Matendo 16

Matendo 16:22-34 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Umati wa watu wakajiunga kuwashambulia Paulo na Sila, na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wapigwe mijeledi. Baada ya kuwapiga sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo. Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. Lakini Paulo akapaza sauti kwa nguvu, akisema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!” Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?” Wakamjibu, “Mwamini Bwana Isa Al-Masihi, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” Wakamwambia neno la Bwana Isa, yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake. Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.

Shirikisha
Soma Matendo 16