Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 14

14
Paulo na Barnaba huko Ikonio
1Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama ilivyokuwa desturi yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu wa Mataifa wakaamini. 2Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini wakawachochea watu wa Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya waumini. 3Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri kuhusu Bwana Isa, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza. 4Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume. 5Watu wa Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe. 6Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo. 7Huko wakaendelea kuhubiri Injili.
Paulo na Barnaba huko Listra
8Katika mji wa Listra, kulikuwa na kiwete, aliyekuwa amelemaa tangu kuzaliwa, na hakuwa ametembea kamwe. 9Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa. 10Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!
11Umati ule wa watu walipoona yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapaza sauti, wakasema kwa lugha yao ya Kilikaonia, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!” 12Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye alikuwa msemaji mkuu. 13Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye na umati ule wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.
14Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema, 15“Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea Habari Njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. 16Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka. 17Lakini hakuacha kuwaonesha watu uwepo wake: Ameonesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.” 18Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuzuia umati ule wa watu kuwatolea dhabihu.
19Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa. 20Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.
Paulo na Barnaba warudi Antiokia ya Siria
21Wakahubiri Injili katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kupitia katika taabu nyingi.” 23Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kundi la waumini wa Isa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana Isa waliyemwamini. 24Kisha wakapitia Pisidia wakafika Pamfilia. 25Baada ya kuhubiri neno la Mungu huko Perga, wakateremkia Atalia.
26Kutoka Atalia wakasafiri baharini wakarudi Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile huduma waliyokuwa wameikamilisha. 27Walipowasili Antiokia wakawaita waumini pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu wa Mataifa. 28Nao wakakaa huko pamoja na wanafunzi kwa muda mrefu.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia