Matendo 13
13
Safari ya kwanza ya Paulo kueneza Injili
(Matendo 13:1–14:28)
Barnaba na Sauli wanatumwa
1Katika kundi la waumini wa Isa huko Antiokia kulikuwa na manabii na walimu: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2Walipokuwa wakimwabudu Mwenyezi Mungu na kufunga, Roho Mtakatifu wa Mungu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi niliyowaitia.” 3Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
Barnaba na Sauli waenda Kipro
4Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho wa Mungu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini hadi kisiwa cha Kipro. 5Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kama msaidizi wao.
6Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu. 7Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu. 8Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho wa Mungu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Mwenyezi Mungu zilizo nyoofu? 11Nawe sasa sikiliza, mkono wa Mwenyezi Mungu u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”
Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akapapasa akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwoneshe njia. 12Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana Isa.
Paulo na Barnaba huko Antiokia ya Pisidia
13Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perga huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko, akarejea Yerusalemu. 14Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi. 15Baada ya Torati ya Musa na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”
16Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu. 17Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile. 18Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani. 19Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba yaliyokuwa yakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao. 20Haya yote yalichukua kama muda wa miaka mia nne na hamsini.
“Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi hadi wakati wa nabii Samweli. 21Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini. 22Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’
23“Kutoka uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Isa, kama alivyoahidi. 24Kabla ya kuja kwa Isa, Yahya alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli. 25Yahya alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’
26“Ndugu zangu, wana wa Ibrahimu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. 27Kwa sababu watu wa Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua, wala kuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. 28Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. 29Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. 30Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. 31Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.
32“Nasi tunawaletea Habari Njema: kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu 33sasa ameyatimiza kwetu sisi, watoto wao, kwa kumfufua Isa, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:
“ ‘Wewe ni Mwanangu;
leo mimi nimekuwa Baba yako.’#13:33 Zaburi 2:7
34Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya:
“ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika
nilizomwahidi Daudi.’#13:34 Isaya 55:3
35Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi,
“ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’#13:35 Zaburi 16:10
36“Basi Daudi alipokwisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa na baba zake, na mwili wake ukaoza. 37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.
38“Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kupitia kwa huyu Isa msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. 39Kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa Torati ya Musa. 40Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:
41“ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka,
mkastaajabu, mkaangamie,
kwa maana nitatenda jambo wakati wenu
ambalo hamtasadiki,
hata kama mtu akiwaambia.’#13:41 Habakuki 1:5”
42Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata. 43Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na watu wa Mataifa walioongokea dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.
44Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Mwenyezi Mungu. 45Lakini Wayahudi walipoona umati ule mkubwa wa watu, walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.
46Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa. 47Kwa maana hili ndilo Mwenyezi Mungu alilotuamuru:
“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa,
ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’#13:47 Isaya 49:6”
48Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Mwenyezi Mungu; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.
49Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote. 50Lakini viongozi wa Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo. 51Hivyo Paulo na Barnaba wakakung’uta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio. 52Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho wa Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.