Matendo 13:26-41
Matendo 13:26-41 NENO
“Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa sababu watu wa Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua, wala kuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu. “Nasi tunawaletea Habari Njema: kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu sasa ameyatimiza kwetu sisi, watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: “ ‘Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.’ Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya: “ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika nilizomwahidi Daudi.’ Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi, “ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’ “Basi Daudi alipokwisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa na baba zake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu. “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kupitia kwa huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. Kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Musa. Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate: “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka, mkastaajabu, mkaangamie, kwa maana nitatenda jambo wakati wenu ambalo hamtasadiki, hata kama mtu akiwaambia.’”