Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 13:26-41

Matendo 13:26-41 Biblia Habari Njema (BHN)

“Ndugu, nyinyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi, wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo. Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe. Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye, kwa siku nyingi, aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. Nasi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: Jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu, amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: ‘Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.’ Na juu ya kumfufua kutoka kwa wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: ‘Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.’ Naam, na katika sehemu nyingine za Zaburi asema: ‘Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.’ Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza matakwa ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza. Kwa hiyo, jueni, ndugu zangu, kwamba kwa njia ya mtu huyu ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu; na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya sheria. Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii: ‘Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.’”

Shirikisha
Soma Matendo 13

Matendo 13:26-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Abrahamu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumwua wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamteremsha kutoka kwa ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hadi Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiria Habari Njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini. Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu. Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu. Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa Torati ya Musa. Angalieni, basi, isiwajie habari ile iliyonenwa katika manabii. Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana.

Shirikisha
Soma Matendo 13

Matendo 13:26-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini. Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu. Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu. Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa. Angalieni, basi, isiwajilie habari ile iliyonenwa katika manabii. Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana.

Shirikisha
Soma Matendo 13

Matendo 13:26-41 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa sababu watu wa Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua, wala kuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu. “Nasi tunawaletea Habari Njema: kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu sasa ameyatimiza kwetu sisi, watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: “ ‘Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.’ Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya: “ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika nilizomwahidi Daudi.’ Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi, “ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’ “Basi Daudi alipokwisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa na baba zake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu. “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kupitia kwa huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. Kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Musa. Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate: “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka, mkastaajabu, mkaangamie, kwa maana nitatenda jambo wakati wenu ambalo hamtasadiki, hata kama mtu akiwaambia.’”

Shirikisha
Soma Matendo 13