Matendo 12
12
Yakobo auawa, Petro atiwa gerezani
1Wakati huo huo Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya waumini wa Isa. 2Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga. 3Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata Petro pia. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. 4Baada ya kumkamata alimfunga gerezani chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka#12:4 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri..
5Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini waumini wa Isa walikuwa wakimwombea kwa Mungu kwa bidii.
6Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda lango la gereza. 7Ghafula malaika wa Mwenyezi Mungu akatokea, na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.
8Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” 9Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. 10Walipita kundi la kwanza la walinzi na la pili, wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo, wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.
11Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.”
12Mara Petro alipotambua hili alienda nyumbani mwa Mariamu, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi. 13Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mjakazi aliyeitwa Roda akaja kumfungulia. 14Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua lango, akapaza sauti, akasema, “Petro yuko langoni!”
15Wakamwambia yule mjakazi, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.”
16Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana. 17Yeye akawaashiria kwa mkono wake wanyamaze kimya, akawaeleza jinsi Mwenyezi Mungu alivyomtoa gerezani. Naye akaongeza kusema, “Waelezeni Yakobo na ndugu wengine habari hizi.” Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine.
18Kulipokucha kukawa na fadhaa kubwa miongoni mwa wale askari kuhusu yaliyomtukia Petro. 19Baada ya Herode kuamuru atafutwe kila mahali na bila kumpata, aliwahoji wale askari walinzi kisha akatoa amri wauawe. Basi Herode Agripa akatoka Yudea akaenda Kaisaria, akakaa huko kwa muda.
Kifo cha Herode Agripa
20Basi Herode Agripa alikuwa amekasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Hivyo watu wa miji hiyo miwili wakaungana pamoja wakataka kukutana naye. Baada ya kuungwa mkono na Blasto, mtumishi maalum wa Mfalme Herode Agripa aliyeaminika, wakaomba mapatano ya amani maana nchi zao zilitegemea nchi ya huyo mfalme kwa mahitaji yao ya chakula.
21Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha utawala, akawahutubia watu. 22Watu waliokuwa wamekusanyika wakapaza sauti, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu!” 23Ghafula, kwa kuwa Herode hakumpa Mungu utukufu, malaika wa Mwenyezi Mungu akampiga, naye akaliwa na chango, akafa.
24Lakini neno la Mungu likaendelea mbele na kuenea, nao wengi wakaambatana nalo.
25Barnaba na Sauli walipomaliza ile huduma yao iliyowapeleka, wakarudi Yerusalemu wakiwa pamoja na Yohana aitwaye Marko.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.