Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:9-23

Matendo 10:9-23 NEN

Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni. Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo. Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.” Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?” Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.