Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:9-23

Matendo 10:9-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.” Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni. Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?” Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.” Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?” Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.” Petro akawakaribisha ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye.

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:9-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inateremshwa kwa pembe zake nne hadi chini; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Inuka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, La, hasha! Bwana, kwa maana sijawahi kula kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Wakati Petro alipokuwa akisumbuka ndani ya nafsi yake, juu ya maana ya maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakatokeza. Walikuwa kukiulizia nyumba ya Simoni, wakiwa wamesimama mbele ya lango, wakaita; wakauliza kama Simoni aitwaye Petro anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi inuka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema, Kornelio jemadari, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, ili asikilize kile utakachosema. Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:9-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako. Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:9-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni. Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo. Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.” Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?” Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.

Shirikisha
Soma Matendo 10