Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wathesalonike 3

3
Hitaji la maombi
1Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana Isa lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu. 2Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini. 3Lakini Bwana Isa ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. 4Nasi tuna tumaini katika Bwana Isa ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. 5Mwenyezi Mungu aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Al-Masihi.
Onyo dhidi ya uvivu
6Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Isa Al-Masihi, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. 7Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. 9Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe mfano wenu wa kufuata. 10Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”
11Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi, bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Isa Al-Masihi, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe. 13Lakini kwenu ninyi, ndugu, kamwe msichoke katika kutenda mema.
14Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyo katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu. 15Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
Salamu za mwisho
16Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Mwenyezi Mungu awe nanyi nyote.
17Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.
18Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe nanyi nyote. Amen.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wathesalonike 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia