Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 6:1-10

2 Samweli 6:1-10 NEN

Tena Daudi akakusanya watu 30,000 wa Israeli waliochaguliwa. Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la BWANA Mwenye Nguvu Zote, ambaye anaketi katika kiti cha enzi kati ya makerubi walioko juu ya hilo Sanduku. Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake. Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za BWANA kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu. Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya BWANA ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza. Daudi akamwogopa BWANA siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la BWANA litakavyoweza kunijia?” Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la BWANA kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti.