2 Samweli 5
5
Daudi atawazwa mfalme wa Israeli
(1 Nyakati 11:1-9; 14:1-7)
1Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako. 2Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Mwenyezi Mungu alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”
3Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Mwenyezi Mungu, nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
4Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini. 5Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu.
Daudi ateka Yerusalemu
6Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” 7Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
8Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”
9Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo#5:9 maana yake Boma la Ngome kuelekea ndani. 10Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikuwa pamoja naye.
11Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. 12Naye Daudi akafahamu kuwa Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake.
13Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake. 14Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, 15Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia, 16Elishama, Eliada na Elifeleti.
Daudi awashinda Wafilisti
(1 Nyakati 14:8-17)
17Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome. 18Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai, 19kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”
Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
20Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, Mwenyezi Mungu amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu#5:20 maana yake Bwana Afurikaye. 21Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua.
22Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai. 23Kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. 24Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” 25Basi Daudi akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba#5:25 Kwa Kiebrania mji huu uliitwa Gibeoni (taz. 1 Nyakati 14:16). hadi Gezeri.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 5: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.