Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 3

3
1Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.
2Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni:
Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;
3mzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli#3:3 au Kileabu mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli;
wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri;
4wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi;
wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;
5wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi.
Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
Abneri amwendea Daudi
6Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli. 7Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake Rispa binti Aya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”
8Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke! 9Mungu na amwadhibu Abneri vikali zaidi ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile Mwenyezi Mungu alichomwahidi kwa kiapo, 10na kuuhamisha ufalme kutoka nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.” 11Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.
12Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”
13Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu hadi umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.” 14Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi mia moja ya Wafilisti.”
15Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi. 16Hata hivyo, mumewe alienda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.
17Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu. 18Sasa fanyeni hivyo! Kwa maana Mwenyezi Mungu alimwahidi Daudi akisema, ‘Kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ”
19Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya. 20Abneri, aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake. 21Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili uweze kutawala yale yote moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.
Yoabu amuua Abneri
22Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani. 23Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme, na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikuwa ameondoka kwa amani.
24Basi Yoabu alienda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa ameenda! 25Unajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza mienendo yako, na kugundua kila kitu unachokifanya.”
26Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili. 27Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa.
28Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za Mwenyezi Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. 29Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha au ukoma, au mwenye kuegemea fimbo, au aangukaye kwa upanga, au kupungukiwa na chakula.”
30(Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)
31Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae gunia, mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza. 32Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.
33Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri:
“Je, ilipasa Abneri afe kama anavyokufa mpumbavu?
34Mikono yako haikufungwa,
miguu yako haikufungwa pingu.
Ulianguka kama yeye aangukaye
mbele ya watu waovu.”
Nao watu wote wakamlilia tena.
35Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi, nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!”
36Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza. 37Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.
38Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mtu mkuu na mashuhuri ameanguka katika Israeli leo? 39Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. Mwenyezi Mungu na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia