Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 2

2
Daudi atiwa mafuta kuwa mfalme wa Yuda
1Ikawa baada ya mambo haya, Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, nipande kwenda katika mojawapo ya miji ya Yuda?”
Mwenyezi Mungu akasema, “Panda.”
Daudi akauliza, “Je, niende wapi?”
Mwenyezi Mungu akajibu, “Nenda Hebroni.”
2Basi Daudi akakwea kwenda huko pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. 3Daudi akawachukua pia watu waliokuwa pamoja naye, kila mmoja na jamaa yake, nao wakaishi huko Hebroni na miji yake. 4Ndipo wanaume wa Yuda wakaja Hebroni, huko wakampaka Daudi mafuta awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.
Daudi alipoambiwa kuwa ni wanaume wa Yabesh-Gileadi waliomzika Sauli, 5akatuma wajumbe kwa wanaume wa Yabesh-Gileadi, kuwaambia, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kuonesha wema huu kwa kumzika Sauli bwana wenu. 6Sasa Mwenyezi Mungu na awaoneshe wema na uaminifu, nami pia nitawaonesha wema ule ule kwa kuwa mmefanya jambo hili. 7Sasa basi, kuweni hodari na mashujaa, kwa maana bwana wenu Sauli amekufa, nao watu wa nyumba ya Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme juu yao.”
Vita kati ya nyumba za Daudi na Sauli
8Wakati huo Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Sauli, alikuwa amemchukua Ish-Boshethi mwana wa Sauli na kumleta hadi Mahanaimu. 9Akamweka awe mfalme juu ya nchi ya Gileadi, Waasheri, Yezreeli, Efraimu, Benyamini na Israeli yote.
10Ish-Boshethi#2:10 maana yake Mtu wa Aibu; pia anaitwa Esh-Baali maana yake Mtu wa Baali (1 Nyakati 8:33; 9:39) mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala Israeli, naye akatawala miaka miwili. Hata hivyo, nyumba ya Yuda ikamfuata Daudi. 11Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ilikuwa miaka saba na miezi sita.
12Abneri mwana wa Neri, pamoja na watumishi wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. 13Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili.
14Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame, wapigane ana kwa ana mbele yetu.”
Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.”
15Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watumishi wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili. 16Kisha kila mwanaume akamkamata mpinzani wake kichwani na kumchoma kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu#2:16 maana yake Uwanja wa Mapambano.
17Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na Waisraeli wakashindwa na watumishi wa Daudi.
18Wana watatu wa Seruya walikuwa huko: Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa. 19Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati alimfuata. 20Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?”
Akamjibu, “Ndiyo.”
21Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana, umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza.
22Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?”
23Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa.
24Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni. 25Ndipo Wabenyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima.
26Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?”
27Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao hadi asubuhi.”
28Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Waisraeli tena, wala hawakuwapiga tena.
29Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu.
30Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watumishi kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea. 31Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua Wabenyamini mia tatu na sitini waliokuwa pamoja na Abneri. 32Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na vijana wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia