Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 3:22-39

2 Samweli 3:22-39 NEN

Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani. Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani. Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda! Wajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.” Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili. Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa. Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za BWANA kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.” (Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.) Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza. Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia. Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri: “Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, miguu yako haikufungwa pingu. Ulianguka kama yeye aangukaye mbele ya watu waovu.” Nao watu wote wakamlilia tena. Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!” Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza. Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri. Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo? Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. BWANA na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”