Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 3:22-39

2 Samueli 3:22-39 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadaye, Yoabu na baadhi ya watu wa Daudi walirudi kutoka mashambulio, wakaleta nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwa pamoja na Daudi huko Hebroni kwani Daudi alikuwa amemuaga aende zake, naye akaondoka kwa amani. Yoabu aliporudi akiwa na jeshi lake lote alilokuwa nalo, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri, alikuwa amekuja kumwona mfalme Daudi, naye amemuaga aende zake, naye ameondoka kwa amani. Yoabu alimwendea mfalme na kumwambia, “Sasa umefanya nini? Tazama Abneri alikuja kwako, kwa nini umemwacha aende? Je, unajua kuwa Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya? Alikuja ili ajue mienendo yako na yale unayoyafanya.” Yoabu alipotoka kuzungumza na Daudi, alituma wajumbe wakamlete Abneri, nao wakamkuta kwenye kisima cha Sira na kumrudisha, lakini Daudi hakujua jambo hilo. Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kwenye lango kana kwamba anataka kuzungumza naye kwa faragha. Hapo Yoabu akamkata Abneri tumboni kwa sababu Abneri alikuwa amemuua Asaheli ndugu yake, na Abneri akafa. Baadaye Daudi aliposikia habari hizo alisema, “Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. Lawama ya mauaji hayo yawe juu ya kichwa cha Yoabu na jamaa yote ya baba yake! Jamaa ya Yoabu daima isikose mtu mwenye ugonjwa wa kisonono, au ugonjwa wa ukoma, au anayetembea kwa magogo au kuuawa kwa upanga, au mwenye kukosa chakula!” Yoabu na ndugu yake Abishai walimuua Abneri kwa kuwa alikuwa amemuua ndugu yao Asaheli wakati wa vita huko Gibeoni. Kisha, mfalme Daudi akamwambia Yoabu na wale wote waliokuwa pamoja naye, wararue mavazi yao, wavae mavazi ya gunia ili wamwombolezee Abneri. Wakati wa mazishi hayo, mfalme Daudi alitembea nyuma ya jeneza. Abneri alizikwa huko Hebroni na mfalme aliomboleza kwa sauti akiwa kando ya kaburi, pia watu wengine wote walifanya vivyo hivyo. Mfalme alimwombolezea Abneri akisema, “Je, ilikuwaje Abneri akafa kama mpumbavu? Mikono yako haikufungwa na miguu yako haikutiwa pingu. Amekufa kama mtu aliyeuawa na waovu!” Na watu wote walimlilia tena. Kisha, watu wote walikwenda kumshawishi Daudi ale mkate wakati ulipokuwa bado mchana. Lakini Daudi aliapa akawaambia, “Mungu na aniue ikiwa nitaonja mkate au kitu chochote hadi jua litakapotua.” Watu wote waliyaona mambo hayo, nao walipendezwa; kama vile kila kitu alichofanya mfalme kilivyowapendeza. Hivyo, siku ile, Waisraeli wote walielewa kwamba haikuwa nia ya mfalme Daudi kumuua Abneri mwana wa Neri. Mfalme Daudi aliwaambia watumishi wake, “Je, hamjui kuwa leo mtu mkuu na mashuhuri amefariki katika Israeli? Ijapokuwa mmenipaka mafuta ili niwe mfalme, lakini leo mimi ni mnyonge. Hawa wana wa Seruya ni wakatili kupita kiasi. Mwenyezi-Mungu na awaadhibu waovu hawa sawasawa na uovu wao.”

2 Samueli 3:22-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta nyara nyingi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake? Wewe unamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akatuma wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hadi katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hadi akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake. Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za BWANA, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri; na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula. Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni. Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata jeneza. Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia. Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia. Wakaja na watu wote wamshurutishe Daudi kula chakula, kukiwa bado mchana; lakini Daudi akaapa, akasema Mungu anitendee vivyo hivyo, na kuzidi, nikionja mkate, au kingine chochote kabla ya jua kutua. Wakaangalia watu wote, yakawa mema machoni pao; kama yalivyokuwa mema machoni pao yote aliyoyatenda mfalme. Wakajua watu wote, na Israeli wote, siku ile, ya kuwa si nia ya mfalme kwamba auawe Abneri, mwana wa Neri. Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, Hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli? Nami leo nimedhoofika, hata nijapotiwa mafuta niwe mfalme; na watu hao, wana wa Seruya, ni wagumu kwangu mimi; BWANA amlipie mwovu kulingana na uovu wake.

2 Samueli 3:22-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta mateka mengi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake? Wewe wamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hata katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hata akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake. Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za BWANA, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri; na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula. Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni. Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata jeneza. Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia. Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia. Wakaja na watu wote wamshurutishe Daudi kula chakula, ukalipo bado mchana; lakini Daudi akaapa, akasema Mungu anitendee vivyo, na kuzidi, nikionja mkate, au kingine cho chote kabla lichwapo jua. Wakaangalia watu wote, yakawa mema machoni pao; kama yalivyokuwa mema machoni pao yote aliyoyatenda mfalme. Wakajua watu wote, na Israeli wote, siku ile, ya kuwa si nia ya mfalme kwamba auawe Abneri, mwana wa Neri. Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, Hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli? Nami leo nimedhoofika, hata nijapotiwa mafuta niwe mfalme; na watu hao, wana wa Seruya, ni wagumu kwangu mimi; BWANA amlipie mwovu sawasawa na uovu wake.

2 Samueli 3:22-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani. Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani. Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda! Wajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.” Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili. Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa. Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za BWANA kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.” (Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.) Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza. Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia. Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri: “Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, miguu yako haikufungwa pingu. Ulianguka kama yeye aangukaye mbele ya watu waovu.” Nao watu wote wakamlilia tena. Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!” Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza. Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri. Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo? Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. BWANA na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”