2 Samweli 3:22-39
2 Samweli 3:22-39 SRUV
Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta nyara nyingi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake? Wewe unamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akatuma wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hadi katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hadi akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake. Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za BWANA, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri; na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula. Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni. Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata jeneza. Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia. Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia. Wakaja na watu wote wamshurutishe Daudi kula chakula, kukiwa bado mchana; lakini Daudi akaapa, akasema Mungu anitendee vivyo hivyo, na kuzidi, nikionja mkate, au kingine chochote kabla ya jua kutua. Wakaangalia watu wote, yakawa mema machoni pao; kama yalivyokuwa mema machoni pao yote aliyoyatenda mfalme. Wakajua watu wote, na Israeli wote, siku ile, ya kuwa si nia ya mfalme kwamba auawe Abneri, mwana wa Neri. Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, Hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli? Nami leo nimedhoofika, hata nijapotiwa mafuta niwe mfalme; na watu hao, wana wa Seruya, ni wagumu kwangu mimi; BWANA amlipie mwovu kulingana na uovu wake.