Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 24

24
Daudi ahesabu wapiganaji
(1 Nyakati 21:1-27)
1Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”
2Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”
3Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”
4Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi; kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.
5Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini mwa mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri. 6Walienda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni. 7Kisha wakaelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walienda Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.
8Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.
9Yoabu akamtolea mfalme idadi ya wapiganaji: Katika Israeli kulikuwa wanaume wenye uwezo elfu mia nane ambao wangeweza kutumia upanga, na katika Yuda watu elfu mia tano.
10Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia Mwenyezi Mungu, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee Mwenyezi Mungu, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
11Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la Mwenyezi Mungu lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema: 12“Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
13Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”
14Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”
15Basi Mwenyezi Mungu akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi hadi muda ulioamriwa, wakafa watu elfu sabini kuanzia Dani hadi Beer-Sheba. 16Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, Mwenyezi Mungu akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Mwenyezi Mungu alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna#24:16 anaitwa Ornani kwa Kiebrania Myebusi.
17Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia Mwenyezi Mungu, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”
Daudi ajenga madhabahu
18Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee Mwenyezi Mungu madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.” 19Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi. 20Arauna alipotazama na kumwona mfalme na maafisa wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme.
21Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?”
Daudi akajibu, “Nimekuja kununua sakafu yako ya kupuria, niweze kumjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”
22Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ng’ombe kwa ajili ya kuni. 23Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na akukubali.”
24Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha! Nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, isiyonigharimu chochote.”
Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha#24:24 Shekeli 50 za fedha ni sawa na gramu 600.. 25Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha Mwenyezi Mungu akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia