Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 17:15-29

2 Samweli 17:15-29 NEN

Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya kadha wa kadha, lakini mimi nimewashauri wao kufanya kadha wa kadha. Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ” Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli, naye mtumishi mmoja wa kike akawa anakwenda kuwapasha habari nao wakawa wanakwenda kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda mpaka kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima katika ua wa nyumba yake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho. Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka kwenye mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo. Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu. Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke haya maji haraka. Ahithofeli ameshauri kadha wa kadha dhidi yako.” Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuwa hajavuka Mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani kwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake. Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na watu wote wa Israeli. Absalomu alikuwa amemweka Amasa juu ya jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwisraeli, ambaye alikuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu. Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi. Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu wakaleta matandiko ya kitandani, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde, asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka kwenye maziwa ya ngʼombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”