Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 17:15-29

2 Samueli 17:15-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari jinsi Ahithofeli na yeye mwenyewe walivyomshauri Absalomu na wazee wa Israeli. Akawaambia wampelekee Daudi habari upesi kwamba asilale usiku kwenye vivuko jangwani, bali, kwa njia yoyote ile, avuke na kuondoka ili asije akakamatwa na kuuawa, yeye pamoja na watu wake wote. Wakati huo, Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakimngojea karibu na Enrogeli, ili wasionekane na mtu yeyote wakiingia mjini. Kila mara mtumishi fulani wa kike alikuwa akiwapelekea habari nao wakaipeleka kwa mfalme Daudi. Lakini wakati huu, walionekana na kijana mmoja ambaye alikwenda na kumhabarisha Absalomu. Hivyo, Yonathani na Ahimaasi waliondoka haraka, wakaenda Bahurimu nyumbani kwa mtu fulani aliyekuwa na kisima uani kwake. Wakaingia humo kisimani na kujificha. Mwanamke mwenye nyumba hiyo akachukua kifuniko na kukifunika kisima hicho, halafu akaanika nafaka juu ya kifuniko. Habari hizo hazikujulikana. Watumishi wa Absalomu walipowasili kwa huyo mwanamke, wakamwambia, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Yule mwanamke akawaambia, “Wamekwenda ngambo ya kijito.” Walipowatafuta na kuwakosa, wakarudi mjini Yerusalemu. Baada ya watumishi wa Absalomu kuondoka, Yonathani na Ahimaasi walitoka kisimani, wakaenda kwa mfalme Daudi na kumpasha habari. Wakamwambia, “Ondoka, uende ngambo ya mto, kwa sababu Ahithofeli amemshauri Absalomu dhidi yako.” Kwa hiyo, Daudi akaondoka na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakavuka mto Yordani. Ilipofika asubuhi hakuna mtu aliyebaki nyuma bila kuvuka mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, alitandika punda wake, akaenda nyumbani, kwenye mji wake. Alipofika huko, alipanga vizuri mambo ya nyumbani kwake, akajinyonga. Akafariki na kuzikwa kwenye kaburi la baba yake. Basi, Daudi akaenda Mahanaimu. Absalomu akavuka mto Yordani na watu wote wa Israeli. Wakati huo, Absalomu alikuwa amemweka Amasa kuwa mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa Yithra, Mwishmaeli. Mama yake aliitwa Abigali binti wa Nahashi, aliyekuwa dada yake, Seruya, mama yake Yoabu. Absalomu pamoja na watu wa Israeli walipiga kambi yao katika nchi ya Gileadi. Daudi alipowasili Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi Mwamoni, kutoka mji wa Raba; Makiri mwana wa Amieli kutoka mji wa Lo-debari, pamoja na Barzilai Mgileadi kutoka mji wa Rogelimu, walipeleka vitanda, mabirika, vyombo vya udongo, ngano, shayiri, unga, bisi, kunde na dengu, asali, siagi, kondoo na jibini kutoka mifugo yao kwa ajili ya Daudi pamoja na watu aliokuwa nao. Maana walisema, “Watu hawa wana njaa, wamechoka na wana kiu kwa ajili ya kusafiri jangwani.”

2 Samueli 17:15-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha. Basi sasa pelekeni habari upesi, kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; ndipo wakamwambie mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake. Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lolote. Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu. Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu. Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki hata mmoja wao asiyevuka Yordani. Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajinyonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye. Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye. Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu. Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi. Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu, wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu, na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng'ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao wanaona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.

2 Samueli 17:15-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha. Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake. Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote. Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu. Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu. Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani. Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye. Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye. Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu. Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi. Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu, wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu, na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng’ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao waona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.

2 Samueli 17:15-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya kadha wa kadha, lakini mimi nimewashauri wao kufanya kadha wa kadha. Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ” Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli, naye mtumishi mmoja wa kike akawa anakwenda kuwapasha habari nao wakawa wanakwenda kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda mpaka kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima katika ua wa nyumba yake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho. Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka kwenye mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo. Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu. Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke haya maji haraka. Ahithofeli ameshauri kadha wa kadha dhidi yako.” Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuwa hajavuka Mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani kwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake. Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na watu wote wa Israeli. Absalomu alikuwa amemweka Amasa juu ya jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwisraeli, ambaye alikuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu. Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi. Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu wakaleta matandiko ya kitandani, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde, asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka kwenye maziwa ya ngʼombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”