Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 16:15-23

2 Samweli 16:15-23 NEN

Wakati huo, Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. Ndipo Hushai, Mwariki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!” Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonyesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?” Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha, yeye aliyechaguliwa na BWANA, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na watu wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye. Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.” Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe shauri lako. Tufanye nini?” Ahithofeli akamjibu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.” Kwa hiyo wakasimika hema kwa ajili ya Absalomu juu ya paa, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake mbele ya Israeli wote. Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.