2 Samueli 16:15-23
2 Samueli 16:15-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati huo, Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. Ndipo Hushai, Mwariki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!” Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonyesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?” Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha, yeye aliyechaguliwa na BWANA, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na watu wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye. Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.” Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe shauri lako. Tufanye nini?” Ahithofeli akamjibu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.” Kwa hiyo wakasimika hema kwa ajili ya Absalomu juu ya paa, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake mbele ya Israeli wote. Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.
2 Samueli 16:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, Absalomu na watu wote wa Israeli wakaenda mjini Yerusalemu na Ahithofeli pamoja nao. Hushai kutoka Arki, rafiki ya Daudi, akamwendea Absalomu, akamwambia, “Uishi mfalme! Uishi mfalme!” Absalomu akamwuliza Hushai, “Je, huu ndio uaminifu wako kwa rafiki yako Daudi? Mbona hukuenda pamoja na rafiki yako?” Hushai akamjibu, “La! Maana yule ambaye amechaguliwa na Mwenyezi-Mungu, watu hawa na watu wote wa Israeli, huyo ndiye, mimi nitakuwa wake yeye, na nitabaki naye. Zaidi ya hayo, je, nitamtumikia nani? Je, si mwana wa rafiki yangu? Basi, kama nilivyomtumikia baba yako ndivyo nitakavyokutumikia wewe.” Ndipo Absalomu alipomwambia Ahithofeli, “Nishauri; tufanye nini?” Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Waingilie masuria wa baba yako ambao aliwaacha kuangalia nyumba yake. Baadaye watu wote wa Israeli watakaposikia kwamba umechukizwa na baba yako, hapo watu wote walio pamoja nawe watatiwa nguvu.” Hivyo, watu wakampigia Absalomu hema kwenye paa, naye akalala na masuria wa baba yake, watu wote wa Israeli wakiwa wanaona. Siku hizo, shauri lolote alilotoa Ahithofeli lilikuwa kama limetolewa na Mungu. Na shauri alilotoa Ahithofeli liliheshimiwa na Daudi na Absalomu.
2 Samueli 16:15-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Absalomu, na hao watu wote wa Israeli, wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. Ikawa, Hushai, Mwarki, rafiki wa Daudi, alipomjia Absalomu, Hushai akamwambia Absalomu, Na aishi mfalme, aishi mfalme. Naye Absalomu akamwambia Hushai, Je! Huu ndio wema wako kwa rafiki yako? Mbona hukutoka pamoja na rafiki yako? Hushai akamwambia Absalomu, La, sivyo; lakini yule aliyechaguliwa na BWANA, na watu hawa, na watu wote wa Israeli, mimi nitakuwa wake, na pamoja naye nitakaa. Na tena, Ni nani ambaye yanipasa nimtumikie? Hainipasi kumtumikia mwanawe? Kama nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mbele yako. Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa ushauri wako, tufanyeje. Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria wa baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. Na ushauri wake Ahithofeli, aliokuwa akiutoa siku zile, ulikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.
2 Samueli 16:15-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Absalomu, na hao watu wote wa Israeli, wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. Ikawa, Hushai, Mwarki, rafiki wa Daudi, alipomjia Absalomu, Hushai akamwambia Absalomu, Na aishi mfalme, aishi mfalme. Naye Absalomu akamwambia Hushai, Je! Huu ndio wema wako kwa rafiki yako? Mbona hukutoka pamoja na rafiki yako? Hushai akamwambia Absalomu, La, sivyo; lakini yule BWANA aliyemchagua, na watu hawa, na watu wote wa Israeli, mimi nitakuwa wake, na pamoja naye nitakaa. Na tena, Ni nani ambaye yanipasa nimtumikie? Hainipasi kutumika mbele ya mwanawe? Kama nilivyotumika mbele ya baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mbele yako. Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje. Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.