Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 15:24-37

2 Samweli 15:24-37 NEN

Sadoki pia alikuwako, kadhalika Walawi wote waliokuwa pamoja naye walikuwa wamechukua Sanduku la Agano la Mungu. Wakaweka chini Sanduku la Mungu, naye Abiathari akatoa dhabihu mpaka watu wote walipokuwa wameondoka mjini. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Rudisha Sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitapata kibali mbele za BWANA, atanirudisha, nami nitaliona Sanduku hili tena pamoja na Maskani yake. Lakini kama yeye atasema, ‘Mimi sipendezwi nawe,’ basi mimi niko tayari; yeye na anifanye chochote aonacho chema kwake.” Pia mfalme alimwambia kuhani Sadoki, “Je, wewe si mwonaji? Rudi mjini kwa amani pamoja na mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari. Wewe na Abiathari wachukueni wana wenu wawili. Nitasubiri kwenye vivuko katika jangwa mpaka neno litakapotoka kwenu kuniarifu.” Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakarudisha Sanduku la Mungu mpaka Yerusalemu na kukaa huko. Bali Daudi akaendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni, akaenda huku analia, akiwa amefunika kichwa chake na bila viatu miguuni. Watu wote waliokuwa pamoja naye nao wakafunika vichwa vyao, wakawa wanapanda mlima huku wanalia. Basi Daudi alikuwa ameambiwa, “Ahithofeli alikuwa miongoni mwa washiriki wa shauri baya la Absalomu.” Ndipo Daudi akaomba, akisema, “Ee BWANA, geuza shauri la Ahithofeli kuwa ujinga.” Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali ambapo watu walikuwa wamezoea kumwabudu Mungu, Hushai, Mwariki, alikuwako huko kumlaki, joho lake likiwa limeraruka na mavumbi kichwani mwake. Daudi akamwambia, “Kama ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. Lakini ikiwa utarudi mjini na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; nilikuwa mtumishi wa baba yako wakati uliopita, lakini sasa nitakuwa mtumishi wako,’ basi utaweza kunisaidia kwa kupinga shauri la Ahithofeli. Je, makuhani Sadoki na Abiathari hawatakuwa pamoja nawe? Waambie lolote utakalosikia katika jumba la mfalme. Wana wao wawili, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao huko. Watume kwangu na lolote utakalosikia.” Kwa hiyo Hushai, rafiki wa Daudi, akafika Yerusalemu wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini.