2 Samueli 15:24-37
2 Samueli 15:24-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Kuhani Abiathari akatoka, hata na kuhani Sadoki akatoka pamoja na Walawi wote huku wamelibeba sanduku la agano la Mungu. Wakaliweka chini lile sanduku la Mungu, mpaka watu wote walipopita kutoka mjini Yerusalemu. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Lirudishe sanduku la agano la Mungu mjini. Kama ninakubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu, bila shaka atanirudisha na kunijalia kuliona tena sanduku lake na kuyaona maskani yake. Lakini ikiwa Mwenyezi-Mungu hapendezwi nami basi, mimi niko tayari; na anitendee lolote analoona jema kwake.” Mfalme Daudi akamwambia tena Sadoki, “Tazama, mchukue mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari mrudi nyumbani kwa amani. Lakini nitakuwa nikingojea penye vivuko huku nyikani, mpaka nitakapopata habari kutoka kwako.” Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakalirudisha sanduku la agano la Mungu mjini Yerusalemu, wakabaki humo. Lakini Daudi aliendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni huku analia, bila viatu na kichwa chake kimefunikwa. Hata watu wote waliokuwa pamoja naye walivifunika vichwa vyao wakawa wanapanda mlima huku wanalia. Wakati huo, Daudi aliambiwa kuwa hata Ahithofeli alikuwa mmoja wa waasi waliojiunga na Absalomu. Lakini Daudi akaomba akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu nakuomba, uufanye mpango wa Ahithofeli usifanikiwe.” Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali pa kumwabudia Mungu, mtu mmoja jina lake Hushai kutoka Arki alikuja ili kumlaki, mavazi yake yakiwa yameraruka na kichwani pake kuna mavumbi. Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. Lakini kama utarudi mjini Yerusalemu na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako, hapo awali’; basi utanifanyia mpango wa Ahithofeli usifanikiwe. Makuhani Sadoki na Abiathari wako pamoja nawe mjini! Basi, chochote utakachosikia kutoka nyumbani kwa mfalme, waambie makuhani Sadoki na Abiathari. Tazama, watoto wao wawili wa kiume, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao. Na chochote mtakachosikia mtanipelekea habari kwa njia yao.” Basi, Hushai rafiki ya mfalme Daudi, akarudi mjini na wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini Yerusalemu.
2 Samueli 15:24-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la Agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hadi watu wote walipokwisha kuutoka mji. Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa BWANA atanirudisha, na kunionesha tena sanduku hili, na maskani yake; lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi, Ahimaasi, mwana wako, na Yonathani, mwana wa Abiathari. Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikia neno la kunipasha habari kutoka kwenu. Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko. Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akapanda huku akilia; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee BWANA, nakusihi, uugeuze ushauri wa Ahithofeli uwe ubatili. Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake likiwa limeraruliwa, tena akiwa na udongo kichwani mwake. Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu; lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu. Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani. Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanitumia habari ya kila neno mtakalolisikia. Basi Hushai, rafiki wa Daudi, akaingia ndani ya mji; naye Absalomu akafika akaingia Yerusalemu.
2 Samueli 15:24-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hata watu wote walipokwisha kuutoka mji. Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa BWANA atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake; lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi, Ahimaasi, mwana wako, na Yonathani, mwana wa Abiathari. Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikilia neno la kunipasha habari kutoka kwenu. Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko. Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee BWANA, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili. Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake. Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu; lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu. Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani. Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanipelekea habari ya kila neno mtakalolisikia. Basi Hushai, rafiki wa Daudi, akaingia ndani ya mji; naye Absalomu akafika akaingia Yerusalemu.
2 Samueli 15:24-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sadoki pia alikuwako, kadhalika Walawi wote waliokuwa pamoja naye walikuwa wamechukua Sanduku la Agano la Mungu. Wakaweka chini Sanduku la Mungu, naye Abiathari akatoa dhabihu mpaka watu wote walipokuwa wameondoka mjini. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Rudisha Sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitapata kibali mbele za BWANA, atanirudisha, nami nitaliona Sanduku hili tena pamoja na Maskani yake. Lakini kama yeye atasema, ‘Mimi sipendezwi nawe,’ basi mimi niko tayari; yeye na anifanye chochote aonacho chema kwake.” Pia mfalme alimwambia kuhani Sadoki, “Je, wewe si mwonaji? Rudi mjini kwa amani pamoja na mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari. Wewe na Abiathari wachukueni wana wenu wawili. Nitasubiri kwenye vivuko katika jangwa mpaka neno litakapotoka kwenu kuniarifu.” Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakarudisha Sanduku la Mungu mpaka Yerusalemu na kukaa huko. Bali Daudi akaendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni, akaenda huku analia, akiwa amefunika kichwa chake na bila viatu miguuni. Watu wote waliokuwa pamoja naye nao wakafunika vichwa vyao, wakawa wanapanda mlima huku wanalia. Basi Daudi alikuwa ameambiwa, “Ahithofeli alikuwa miongoni mwa washiriki wa shauri baya la Absalomu.” Ndipo Daudi akaomba, akisema, “Ee BWANA, geuza shauri la Ahithofeli kuwa ujinga.” Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali ambapo watu walikuwa wamezoea kumwabudu Mungu, Hushai, Mwariki, alikuwako huko kumlaki, joho lake likiwa limeraruka na mavumbi kichwani mwake. Daudi akamwambia, “Kama ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. Lakini ikiwa utarudi mjini na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; nilikuwa mtumishi wa baba yako wakati uliopita, lakini sasa nitakuwa mtumishi wako,’ basi utaweza kunisaidia kwa kupinga shauri la Ahithofeli. Je, makuhani Sadoki na Abiathari hawatakuwa pamoja nawe? Waambie lolote utakalosikia katika jumba la mfalme. Wana wao wawili, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao huko. Watume kwangu na lolote utakalosikia.” Kwa hiyo Hushai, rafiki wa Daudi, akafika Yerusalemu wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini.