2 Samweli 12:24-31
2 Samweli 12:24-31 NEN
Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina lake Solomoni. BWANA alimpenda Solomoni. Kwa kuwa BWANA alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia kwa ajili ya BWANA. Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome la kifalme. Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji. Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.” Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka. Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.