2 Samueli 12:24-31
2 Samueli 12:24-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda; akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya BWANA. Yoabu akapigana juu mji wa Waamoni, akautwaa mji wa kifalme. Yoabu akatuma wajumbe waende kwa Daudi, kusema Nimeshindana na Raba, hata nimeutwaa huo mji wa maji. Basi sasa kusanya watu waliobaki, ukauzunguke mji, na kuutwaa; nisije mimi nikautwaa mji, ukaitwe jina langu. Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa. Kisha akamnyang'anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nalo lilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana. Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya misumeno, na sululu za chuma, na mashoka ya chuma, akawafanyiza kazi tanurini mwa matofali; ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.
2 Samueli 12:24-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina lake Solomoni. BWANA alimpenda Solomoni. Kwa kuwa BWANA alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia kwa ajili ya BWANA. Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome la kifalme. Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji. Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.” Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka. Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
2 Samueli 12:24-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu Daudi akamfariji Bathsheba mkewe. Akalala naye, naye akapata mimba na kujifungua mtoto wa kiume, ambaye Daudi alimwita Solomoni. Mwenyezi-Mungu alimpenda mtoto huyo, naye akamtuma nabii Nathani kwa Daudi kuwa amwite mtoto huyo Yedidia kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo, Yoabu aliushambulia Raba mji wa Waamoni, naye akauteka huo mji wa kifalme. Yoabu akatuma ujumbe kwa Daudi, “Nimeushambulia mji wa Raba, nami nimelikamata bwawa lao la maji. Sasa wakusanye watu wote waliosalia, upige kambi kuuzunguka na kuuteka. La sivyo, nikiuteka, utaitwa kwa jina langu.” Hivyo, Daudi akakusanya watu wote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka mji huo. Kisha akachukua taji ya mfalme wao kutoka kichwani pake. Uzito wa taji hiyo ya dhahabu ulikuwa kilo thelathini na tano; na ndani yake mlikuwamo jiwe la thamani. Naye Daudi akavikwa taji hiyo kichwani pake. Pia aliteka idadi kubwa sana ya nyara katika mji huo. Halafu aliwachukua watu wa mji huo, akawaweka wafanye kazi wakitumia misumeno, sururu za chuma, mashoka ya chuma na kuwatumia kufanya kazi katika tanuri ya matofali; hivyo ndivyo alivyoitenda miji yote ya Waamoni. Hatimaye Daudi na watu wote walirudi Yerusalemu.
2 Samueli 12:24-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Daudi akamfariji Bath-sheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda; akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya BWANA. Yoabu akapigana juu ya Raba wa wana wa Amoni, akautwaa mji wa kifalme. Yoabu akatuma wajumbe waende kwa Daudi, kusema Nimeshindana na Raba, hata nimeutwaa huo mji wa maji. Basi sasa kusanya watu waliobaki, ukauzunguke mji, na kuutwaa; nisije mimi nikautwaa mji, ukaitwe jina langu. Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa. Kisha akamnyang’anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nayo ilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana. Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya misumeno, na sululu za chuma, na mashoka ya chuma, akawatumikisha tanuuni mwa matofali; ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.