2 Petro 2
2
Walimu wa uongo na uangamizi wao
1Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana Mungu Mwenyezi wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. 2Nao wengi watafuata njia zao potovu, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. 3Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.
4Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa Kuzimu#2:4 Kuzimu hapa linalotokana na neno Tartarus la Kiyunani; maana yake ni kule ndani sana katika mahali pa mateso kwa watu waliopotea. katika vifungo vya giza wakae humo hadi ije hukumu; 5kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, lakini akamhifadhi Nuhu, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7na kama alimwokoa Lutu, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8(kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9ikiwa hivyo ndivyo, basi Mwenyezi Mungu anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. 10Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.
Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni. 11Lakini hata malaika, ijapokuwa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Mwenyezi Mungu. 12Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.
13Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki karamu pamoja nanyi. 14Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! 15Wameiacha njia iliyo nyoofu, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. 16Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, alipoongea kwa sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.
17Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu unaopeperushwa na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18Kwa maana wao hunena maneno matupu ya kiburi. Nao wanavutia tamaa mbaya za asili ya mwili, ili kuwashawishi watu ambao wanajiondoa kutoka kwa wale wanaoishi katika hatia. 19Wanawaahidi uhuru wakati wao wenyewe ni watumwa wa upotovu; kwa maana “mtu ni mtumwa wa chochote kinachomtawala.” 20Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Isa Al-Masihi, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya kuliko ile ya kwanza. 21Ingekuwa afadhali kwao kama hawangeijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22Kwao mithali zimetukia kuwa za kweli, zinaposema: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,”#2:22 Mithali 26:11 tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
Iliyochaguliwa sasa
2 Petro 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.