2 Petro 1
1
Salamu
1Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Isa Al-Masihi.
Kwa wale ambao kupitia kwa haki ya Mungu na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu.
2Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Isa Bwana wetu.
Wito wa Mfuasi wa Al-Masihi na uteule
3Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; 7katika utauwa, upendano wa kindugu; na katika upendano wa kindugu, upendo. 8Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yatawasaidia kutokosa bidii wala kutokuzaa matunda katika kumjua Bwana wetu Isa Al-Masihi. 9Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya, haoni mbali na ni kipofu, naye amesahau kwamba ametakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
Unabii wa Maandiko
12Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo. 13Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niko katika hema hili ambalo ni mwili wangu, 14kwa sababu najua kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Isa Al-Masihi alivyoliweka wazi kwangu. 15Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
16Tulipowafahamisha kuhusu uweza na kuja kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake. 17Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba#1:17 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.”#1:17 Mathayo 17:5; Marko 9:7; Luka 9:35 18Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
19Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama nuru inavyong’aa gizani, hadi kupambazuke na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
2 Petro 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.