Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 5:1-14

2 Wafalme 5:1-14 NEN

Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, BWANA alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari shujaa, lakini alikuwa na ukoma. Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimekwenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angelimwona nabii aliyeko Samaria! Angemponya ukoma wake.” Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli. Mfalme wa Aramu akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumi za fedha, shekeli 6,000 za dhahabu, na mivao kumi ya mavazi. Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.” Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!” Elisha mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi zake na magari yake, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha. Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.” Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la BWANA Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu. Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wafalme 5:1-14

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha