Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 5:1-14

2 Wafalme 5:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi. Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami. Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Nenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nilidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.

2 Wafalme 5:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, BWANA alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari shujaa, lakini alikuwa na ukoma. Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimekwenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angelimwona nabii aliyeko Samaria! Angemponya ukoma wake.” Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli. Mfalme wa Aramu akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumi za fedha, shekeli 6,000 za dhahabu, na mivao kumi ya mavazi. Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.” Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!” Elisha mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi zake na magari yake, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha. Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.” Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la BWANA Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu. Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

2 Wafalme 5:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Naamani, kamanda wa jeshi la mfalme wa Aramu alikuwa mtu mashuhuri aliyependwa sana na bwana wake, kwani kwa njia yake Mwenyezi-Mungu aliiletea nchi ya Aramu ushindi. Alikuwa askari hodari, lakini alikuwa na ugonjwa wa ukoma. Katika vita walivyokuwa wakipigana na Israeli, Waaramu walikuwa wamemchukua msichana mmoja mdogo kutoka Israeli, naye akawa anamtumikia mke wa Naamani. Siku moja akamwambia bibi yake, mke wa Naamani, “Laiti bwana wangu angekwenda na kumwona yule nabii aliyeko Samaria! Angemponya ugonjwa wake.” Naamani alipopata habari hizi, akaenda kwa mfalme na kumweleza habari za mtoto huyu. Mfalme wa Aramu akamwambia, “Chukua barua hii umpelekee mfalme wa Israeli.” Hivyo Naamani akaondoka, huku amechukua vipande 30,000 vya fedha, vipande 6,000 vya dhahabu na mavazi kumi ya sikukuu. Barua yenyewe iliandikwa hivi, “Barua hii ni ya kumtambulisha kwako ofisa wangu Naamani. Nataka umtibu huu ugonjwa wake.” Mfalme wa Israeli aliposoma barua hii alirarua mavazi yake na kusema, “Mbona mfalme wa Aramu anataka nimtibu mtu huyu ukoma wake? Kwani anafikiri mimi ni Mungu aliye na uwezo wa kuua au kufufua? Fahamuni basi, mwone ya kwamba mtu huyu anataka kuniletea mzozo.” Elisha, nabii wa Mungu, alipopata habari kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, alituma ujumbe kwa mfalme, akamwuliza, “Mbona umeyararua mavazi yako? Mlete mtu huyo kwangu, ili apate kujua kwamba kuna nabii katika Israeli?” Naamani akaenda na farasi wake na gari lake mpaka mlangoni mwa Elisha. Elisha akamtuma mtumishi wake amwambie, “Nenda ukaoge mara saba mtoni Yordani, nawe utapona kabisa.” Lakini Naamani alikasirika sana, akaenda zake akisema, “Nilidhani kwamba hakika atanijia na kumwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, apitishe mikono yake juu ya mahali ninapougua na kuniponya! Isitoshe, je, mito Abana na Farpari ya huko Damasko si bora kuliko mito yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga humo na kupona?” Akaondoka na kurudi nyumbani, huku amekasirika sana. Watumishi wake wakamwendea na kumwambia, “Baba yetu kama nabii angekuambia ufanye jambo fulani gumu, je, hungelifanya? Sasa, aliyokuambia tu ni: ‘Jioshe, ili upone!’” Basi, Naamani akateremka mtoni Yordani akajitumbukiza humo mara saba, kama alivyoagizwa na Elisha mtu wa Mungu, naye akapona kabisa. Ngozi yake ikawa imara na yenye afya kama ya mtoto mdogo.

2 Wafalme 5:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi. Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami. Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha