Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 3:13-27

2 Wafalme 3:13-27 NENO

Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.” Mfalme wa Israeli akajibu, “La, sivyo, kwa sababu ni BWANA ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.” Elisha akasema, “Hakika kama BWANA wa majeshi aishivyo, ninayemtumikia, kama si kwa heshima niliyo nayo kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.” Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa BWANA ukaja juu ya Elisha, naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’ Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ngʼombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa. Hili ni jambo rahisi machoni pa BWANA. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu. Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.” Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji. Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani. Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu. Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!” Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga hata wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu. Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri hadi likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia. Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu mia saba wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa. Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.