Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 3:13-27

2 Wafalme 3:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Elisha akamwuliza mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda ukawatake shauri manabii ambao baba yako na mama yako waliwaendea.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Sivyo! Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetuita sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” Elisha akasema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu ambaye mimi ninamtumikia, naapa kwamba kama isingekuwa kwa heshima niliyo nayo kwa rafiki yako mfalme Yehoshafati wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. Lakini sasa niletee mpiga kinanda.” Wakamletea mpiga kinanda. Ikawa alipopiga kinanda, nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elisha, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Chimbeni mashimo kila mahali kote bondeni. Ingawa hamtaona upepo wala mvua, bonde litajaa maji, nanyi mtakunywa, nyinyi pamoja na ng'ombe wenu na wanyama wenu.’ Lakini hili si jambo gumu kwa Mwenyezi-Mungu; yeye atawapeni pia ushindi juu ya Moabu. Mtashinda kila mji wenye ngome na kila mji mzuri; mtaikata miti yao yote, mtaziba chemchemi zote za maji, na kuyaharibu mashamba yao yote yenye rutuba kwa kuyajaza mawe.” Kesho yake asubuhi, wakati wa kutambikia, maji yakatiririka kutoka upande wa Edomu na kujaa kila mahali bondeni. Wamoabu walipopata habari kwamba hao wafalme watatu wamekuja kuwashambulia, watu wote wawezao kuvaa silaha kuanzia vijana mpaka wazee, waliitwa, wakapewa silaha na kuwekwa mpakani tayari kwa vita. Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu. Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!” Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka. Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu. Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao.

2 Wafalme 3:13-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe. Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake. Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki. Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng'ombe zenu, na wanyama wenu. Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu. Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe. Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji. Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani. Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likametameta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu. Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana wenyewe kwa wenyewe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo! Hata walipokuja kambini mwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga Wamoabi hadi kwao. Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.

2 Wafalme 3:13-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe. Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake. Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki. Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng’ombe zenu, na wanyama wenu. Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu. Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe. Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji. Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani. Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likameta-meta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu. Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana kila mtu na mwenziwe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo! Hata walipokuja matuoni kwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga-piga Wamoabi hata kwao. Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.

2 Wafalme 3:13-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina nini mimi nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.” Mfalme wa Israeli akajibu, “La hasha, kwa sababu ni BWANA ambaye ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.” Elisha akasema, “Hakika, kama BWANA Mwenye Nguvu Zote aishivyo ambaye ninamtumikia, kama si kuheshimu Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekutazama wala hata kukutupia jicho. Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.” Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa BWANA ukaja juu ya Elisha, naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’ Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ngʼombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa. Hili ni jambo rahisi machoni pa BWANA. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu. Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.” Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji. Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani. Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu. Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!” Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga mpaka wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu. Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri mpaka likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia vilevile. Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu 700 wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa. Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.