2 Wafalme 25
25
Kuanguka kwa Yerusalemu
(2 Nyakati 36:13-21; Yeremia 52:3-30)
1Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote. 2Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia. 3Ilipofika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 4Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 5Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 6naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, ambapo hukumu yake ilitangazwa. 7Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayang’oa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
8Siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 9Alichoma moto Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 10Jeshi lote la Wakaldayo, chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu. 11Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. 12Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
13Wakaldayo walivunja vipande vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli. 14Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. 15Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
16Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika. 17Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane#25:17 Dhiraa 18 ni sawa na mita 8.2.. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu#25:17 Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35. na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.
18Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. 19Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. 20Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. 21Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.
Hivyo Yuda wakaenda utumwani mbali na nchi yao.
22Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda. 23Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kuwa mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 24Gedalia akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.”
25Hata hivyo, katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi, nao wakamuua Gedalia, na pia watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa naye huko Mispa. 26Baada ya haya, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo.
Yehoyakini anaachiwa
(Yeremia 52:31-34)
27Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki#25:27 au Ameli-Mariduki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili. 28Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kuliko wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli. 29Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme. 30Siku kwa siku mfalme alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wafalme 25: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.