Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 25:13-21

2 Wafalme 25:13-21 NENO

Wakaldayo walivunja vipande vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli. Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha. Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza. Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani mbali na nchi yao.