2 Wafalme 21:16-26
2 Wafalme 21:16-26 NEN
Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa BWANA. Matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Manase akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake. Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba. Akatenda maovu machoni mwa BWANA, kama baba yake Manase alivyofanya. Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. Akamwacha BWANA, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za BWANA. Watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, nao wakamuulia kwake nyumbani. Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake. Matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.