2 Wafalme 21:16-26
2 Wafalme 21:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Zaidi ya hayo, licha ya dhambi yake alipowakosesha watu wa Yuda wakafanya dhambi kwa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Manase aliwaua watu wengi wasiokuwa na hatia, damu ilijaa toka upande mmoja mpaka upande mwingine wa Yerusalemu. Matendo mengine ya Manase na yote aliyotenda, pamoja na dhambi zake zote, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Manase alifariki na kuzikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, katika Bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akatawala mahali pake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu. Jina la mama yake ni Meshulemethi, binti Haruzi wa Yothba. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya. Alifuata njia yote aliyoiendea baba yake na kutumikia sanamu ambazo baba yake alizitumikia na kuziabudu. Alimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hakushika njia ya Mwenyezi-Mungu. Baadaye watumishi wa Amoni walikula njama na kumwua katika ikulu yake. Lakini watu wa Yuda wakawaua wote waliomuua Amoni. Kisha watu hao wa Yuda wakamtawaza Yosia mwanawe mahali pake. Matendo mengine yote ya Amoni yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda. Amoni alizikwa kaburini katika bustani ya Uza; na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 21:16-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka miwili huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Meshulemethi, binti Haruzi wa Yotba. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kama Manase babaye alivyofanya. Akaiendea njia yote aliyoiendea baba yake, akazitumikia sanamu alizozitumikia baba yake, akaziabudu. Akamwacha BWANA, Mungu wa babaze, wala hakuiendea njia ya BWANA. Nao watumishi wa Amoni wakamfitinia, wakamwua mfalme ndani ya nyumba yake mwenyewe. Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliomfitinia mfalme Amoni, watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme mahali pake. Basi mambo yote ya Amoni yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Akazikwa kaburini mwake katika bustani ya Uza. Na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 21:16-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka miwili huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Meshulemethi, binti Haruzi wa Yotba. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kama Manase babaye alivyofanya. Akaiendea njia yote aliyoiendea baba yake, akazitumikia sanamu alizozitumikia baba yake, akaziabudu. Akamwacha BWANA, Mungu wa babaze, wala hakuiendea njia ya BWANA. Nao watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, wakamwua mfalme ndani ya nyumba yake mwenyewe. Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliofanya fitina juu yake mfalme Amoni, watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme mahali pake. Basi mambo yote ya Amoni yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Akazikwa kaburini mwake katika bustani ya Uza. Na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 21:16-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa BWANA. Matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Manase akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake. Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba. Akatenda maovu machoni mwa BWANA, kama baba yake Manase alivyofanya. Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. Akamwacha BWANA, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za BWANA. Watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, nao wakamuulia kwake nyumbani. Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake. Matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.