2 Wafalme 2:1-12
2 Wafalme 2:1-12 NEN
Wakati BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali. Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. BWANA amenituma Betheli.” Lakini Elisha akasema, “Kwa hakika, kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja. Wana wa manabii waliokuwako huko Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. BWANA amenituma Yeriko.” Naye akajibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko. Wana wa manabii waliokuwako huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. BWANA amenituma kwenda Yordani.” Naye akamjibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja. Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama kando ya Mto Yordani. Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu. Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.” Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hautalipata.” Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzirarua.