2 Wafalme 2:1-12
2 Wafalme 2:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Ikawa wakati ulipofika ambapo Mwenyezi-Mungu alitaka kumchukua Elia mbinguni katika upepo wa kisulisuli, Elia na Elisha walikuwa njiani, wakitoka Gilgali. Baadaye walipokuwa njiani, Elia alimwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Betheli.” Lakini Elisha akamwambia, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo, sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja hadi Betheli. Wanafunzi wa manabii waliokuwa huko wakamwendea Elisha, wakamwuliza, “Je, unajua kwamba leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Yeriko.” Lakini Elisha akakataa akisema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja mpaka Yeriko. Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja. Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo. Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu. Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.” Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.” Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli. Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia. Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili.
2 Wafalme 2:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, hapo BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Betheli. Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko. Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lolote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
2 Wafalme 2:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, hapo BWANA alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Betheli. Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko. Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
2 Wafalme 2:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali. Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. BWANA amenituma Betheli.” Lakini Elisha akasema, “Kwa hakika, kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja. Wana wa manabii waliokuwako huko Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. BWANA amenituma Yeriko.” Naye akajibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko. Wana wa manabii waliokuwako huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. BWANA amenituma kwenda Yordani.” Naye akamjibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja. Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama kando ya Mto Yordani. Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu. Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.” Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hautalipata.” Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzirarua.