2 Wakorintho 4
4
Hazina ya mbinguni katika vyombo vya udongo
1Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa. 2Lakini tumekataa mambo ya siri na ya aibu; hatufuati njia za udanganyifu, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. 3Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Al-Masihi, aliye sura ya Mungu. 5Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe, ila tunamhubiri Isa Al-Masihi kuwa ni Bwana, na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Isa. 6Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ing’ae gizani,”#4:6 Mwanzo 1:3 ameifanya nuru yake ing’ae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Al-Masihi.
7Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu, wala si kwetu. 8Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Isa ili uzima wa Isa uweze kudhihirishwa katika miili yetu. 11Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Isa, ili uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. 12Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.
13Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.”#4:13 Zaburi 116:10 Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema, 14kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia pamoja na Isa na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake. 15Haya yote ni kwa faida yenu, ili neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.
16Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi. 18Kwa hivyo hatuangalii yale yanayoonekana, bali yale yasiyoonekana. Kwa maana yale yanayoonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoonekana ni ya milele.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.