Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 3

3
Wahudumu wa agano jipya
1Je, tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji kupata barua za utambulisho kwenu au kutoka kwenu, kama watu wengine? 2Ninyi wenyewe ndio barua yetu iliyoandikwa katika mioyo yetu, inayojulikana na kusomwa na kila mtu. 3Nanyi mwadhihirisha wazi kwamba ninyi ni barua inayotoka kwa Al-Masihi, matokeo ya huduma yetu, ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya wanadamu.
4Hili ndilo tumaini tulilo nalo mbele za Mungu kupitia kwa Al-Masihi. 5Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lolote wenyewe, lakini utoshelevu wetu unatoka kwa Mungu. 6Ndiye alitutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya: si wa andiko, bali wa Roho wa Mungu; kwa kuwa andiko huua, bali Roho hutia uzima.
Utukufu wa agano jipya
7Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe, ilikuja kwa utukufu hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Musa kwa sababu ya ule utukufu wake, ingawa ulikuwa wa kufifia, 8je, huduma ya Roho wa Mungu haitakuwa na utukufu zaidi? 9Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi? 10Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu, kikilinganishwa na huu utukufu unaozidi. 11Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu!
12Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana. 13Sisi si kama Musa, ambaye ilimpasa kuweka utaji wa kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mng’ao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka. 14Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana hadi leo utaji ule ule hufunika Torati inaposomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Al-Masihi peke yake unaondolewa. 15Hata leo Torati ya Musa inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. 16Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana Mungu Mwenyezi, utaji unaondolewa. 17Basi Bwana Isa ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi, hapo pana uhuru. 18Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji, tunadhihirisha utukufu wa Bwana Isa kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, unaotoka kwa Bwana Isa, aliye Roho.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wakorintho 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia