Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 1

1
Salamu
1Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu.
Kwa kundi la waumini wa Mungu walioko Korintho, pamoja na watakatifu wote walio nchi ya Akaya yote.
2Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba#1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Mungu wa faraja yote
3Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5Kama vile mateso ya Al-Masihi yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Al-Masihi. 6Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu.
8Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko jimbo la Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. 9Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10Yeye ametuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo, na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa, 11kama vile mnavyoungana kusaidiana nasi katika maombi. Hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.
Paulo aahirisha ziara
12Basi haya ndio majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu kwa utakatifu na uaminifu unaotoka kwa Mungu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu. 13Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba, 14kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Isa.
15Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili. 16Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Yudea. 17Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?
18Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajakuwa “Ndiyo” na “Siyo”. 19Kwa kuwa Isa Al-Masihi, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silvano#1:19 yaani Sila, na Timotheo tulimhubiri kwenu, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo”, bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo”. 20Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Al-Masihi ni “Ndiyo”. Kwa sababu hii, ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu. 21Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Al-Masihi. Alitupaka mafuta 22kwa kututia muhuri wake na kutupatia Roho wake Mtakatifu mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia yote aliyotuahidi.
23Namwita Mungu awe shahidi wangu kwamba sikurudi Korintho kwa sababu niliwahurumia ninyi. 24Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi ili mfurahi, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wakorintho 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia