Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 22

22
Ahazia mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 8:25-29; 9:21-28)
1Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula walioingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala.
2Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri.
3Ahazia naye akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, kwa sababu mama yake alimshawishi kutenda uovu. 4Akafanya yaliyo maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake, nyumba ya Ahabu ndio walikuwa washauri wake, kwa uangamivu wake. 5Pia akafuata ushauri wao alipoenda pamoja na Yoramu#22:5 au Yehoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. 6Hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa huko Ramothi#22:6 Rama kwa Kiebrania. alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.
Ndipo Ahazia#22:6 au Azaria mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.
7Mungu alisababisha anguko la Ahazia kutokana na Ahazia kwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye Mwenyezi Mungu alikuwa amempaka mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu. 8Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua. 9Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamuua. Wakamzika, kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Mwenyezi Mungu kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme.
Athalia na Yoashi
(2 Wafalme 11:1-3)
10Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme ya nyumba ya Yuda. 11Lakini Yehosheba, binti Mfalme Yehoramu, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala. Kwa kuwa Yehosheba, aliyekuwa binti Mfalme Yehoramu, na pia alikuwa mke wa kuhani Yehoyada, alikuwa dada yake Ahazia, akamficha huyo mtoto ili Athalia asimuue. 12Alibaki amefichwa pamoja nao katika Hekalu la Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia