2 Nyakati 21
21
Yehoramu mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 8:17-24)
1Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake. 2Ndugu zake Yehoramu, wana wa Yehoshafati walikuwa: Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli na Shefatia. Hawa wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli#21:2 yaani Yuda.. 3Baba yao alikuwa amewapa zawadi nyingi za fedha na dhahabu na vitu vya thamani, pamoja na miji yenye ngome huko Yuda, bali akampa Yehoramu ufalme kwa sababu alikuwa mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.
4Baada ya Yehoramu kujiimarisha katika ufalme wa baba yake, akawaua kwa upanga ndugu zake wote pamoja na baadhi ya wakuu wa Israeli. 5Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka nane. 6Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. 7Hata hivyo, kwa sababu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amefanya na Daudi, Mwenyezi Mungu hakuwa radhi kuangamiza nyumba ya Daudi. Mungu alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili yake na wazao wake milele.
8Wakati wa utawala wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe. 9Basi Yehoramu akaenda huko pamoja na maafisa wake na magari yake ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. 10Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda.
Libna pia wakaasi wakati huo huo kwa sababu Yehoramu alikuwa amemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake. 11Alikuwa pia ametengeneza mahali pa juu pa kuabudia katika vilima vya Yuda na akawa amewasababisha watu wa Yerusalemu kufanya uzinzi na akawa amewapotosha watu wa Yuda.
12Yehoramu akapokea barua kutoka kwa nabii Ilya iliyosema:
“Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Daudi baba yako, asemalo: ‘Hukuenenda katika njia za Yehoshafati baba yako au za Asa mfalme wa Yuda. 13Lakini umeenenda katika njia za wafalme wa Israeli, nawe umewaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu kuzini, kama vile nyumba ya Ahabu ilivyofanya. Pia umewaua ndugu zako mwenyewe, watu wa nyumbani mwa baba yako, watu waliokuwa bora kuliko wewe. 14Hivyo basi Mwenyezi Mungu yu karibu kuwapiga watu wako, wanao, wake zako na kila kitu kilicho chako, kwa pigo zito. 15Wewe mwenyewe utaugua sana kwa ugonjwa wa tumbo kwa muda mrefu, hadi ugonjwa utakaposababisha matumbo yako kutoka nje.’ ”
16Mwenyezi Mungu akaamsha chuki ya Wafilisti na ya Waarabu walioishi karibu na Wakushi dhidi ya Yehoramu. 17Wakaishambulia Yuda, wakaivamia na kuchukua mali yote iliyopatikana katika jumba la mfalme pamoja na wanawe na wake zake. Hakubakiziwa mwana yeyote isipokuwa Ahazia aliyekuwa mdogo wa wote.
18Baada ya mambo haya yote, Mwenyezi Mungu akampiga Yehoramu kwa ugonjwa wa matumbo usio wa kupona. 19Ikawa baada ya muda, mwisho wa mwaka wa pili, matumbo yake yakatoka nje kwa sababu ya ugonjwa, naye akafa katika maumivu makali sana. Watu wake hawakuwasha moto kwa heshima yake, kama walivyokuwa wamewafanyia baba zake.
20Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipokuwa mfalme, naye akatawala huko Yerusalemu miaka nane. Akafa, bila kusikitikiwa na mtu yeyote, naye akazikwa katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
Iliyochaguliwa sasa
2 Nyakati 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.