Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 18:8-27

2 Nyakati 18:8-27 NEN

Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.” Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo BWANA asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ” Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho, wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.” Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.” Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, nitamwambia kile tu BWANA atakachoniambia.” Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa watatiwa mkononi mwako.” Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la BWANA?” Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye BWANA akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ” Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu bali mabaya tu?” Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la BWANA: Nilimwona BWANA ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama upande wa kulia na wa kushoto. Naye BWANA akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu, mfalme wa Israeli, ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile. Mwishoni, roho akajitokeza, akasimama mbele za BWANA na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “BWANA akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “BWANA akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’ “Kwa hiyo sasa BWANA ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. BWANA ameamuru maafa kwa ajili yako.” Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa BWANA alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?” Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.” Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme. Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ” Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi BWANA hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha