Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 18:8-27

2 Mambo ya Nyakati 18:8-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli akamwita ofisa mmoja na kumwamuru, “Haraka, nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati, mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme. Wakati huo manabii wote walikuwa wakitoa unabii wao mbele yao. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Washamu hata kuwaangamiza.’” Hata wale manabii wengine wakatabiri vivyo hivyo wakasema, “Nenda ukaushambulie Ramoth-gileadi, Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Wakati huo, yule mjumbe aliyetumwa kwa Mikaya alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” Lakini Mikaya akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, kile atakachoniambia Mungu wangu, ndicho nitakachosema.” Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme akamwuliza, “Je, twende kupigana vitani huko Ramoth-gileadi au nisiende?” Mikaya akajibu, “Nenda ushinde; Mwenyezi-Mungu atawatia mikononi mwako.” Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba kila unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” Naye Mikaya akasema, “Niliwaona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; waache warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’” Hapo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia, kamwe hatatabiri jema juu yangu, ila mabaya tu?” Kisha Mikaya akasema: “Haya, sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lake lote la mbinguni limesimama upande wake wa kulia na wa kushoto. Ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu mfalme wa Israeli aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. Kisha, pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya nenda ukafanye hivyo.’ Basi ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako waseme uongo. Lakini Bwana amenena mabaya juu yako!” Hapo nabii Sedekia mwana wa Kenaana akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Kwa njia gani Roho wa Mwenyezi-Mungu ameniacha na akaja kunena nawe?” Mikaya akamjibu, “Siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha ndipo utakapojua.” Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi, mwana wa mfalme. Waambie wamfunge gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama, basi, utajua Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikieni, enyi watu wote!”

2 Mambo ya Nyakati 18:8-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo mfalme wa Israeli akamwita kamanda mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Sedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia. Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kupatana yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Niliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nilimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kulia na wa kushoto. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kufanikiwa pia; ondoka, ukafanye hivyo. Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako. Ndipo akakaribia Sedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu Roho ya BWANA ili aseme na wewe? Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hadi nitakaporudi kwa amani. Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kupitia kwangu. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

2 Mambo ya Nyakati 18:8-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye sakafu pa kuingilia lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia. Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo. Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako. Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya BWANA ili aseme na wewe? Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

2 Mambo ya Nyakati 18:8-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.” Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo BWANA asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ” Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho, wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.” Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.” Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, nitamwambia kile tu BWANA atakachoniambia.” Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa watatiwa mkononi mwako.” Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la BWANA?” Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye BWANA akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ” Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu bali mabaya tu?” Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la BWANA: Nilimwona BWANA ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama upande wa kulia na wa kushoto. Naye BWANA akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu, mfalme wa Israeli, ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile. Mwishoni, roho akajitokeza, akasimama mbele za BWANA na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “BWANA akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “BWANA akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’ “Kwa hiyo sasa BWANA ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. BWANA ameamuru maafa kwa ajili yako.” Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa BWANA alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?” Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.” Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme. Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ” Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi BWANA hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”