Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 4

4
1Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote.
Wafilisti wateka Sanduku la Mungu
Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki. 2Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita. 3Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.”
4Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, walikuwa huko na Sanduku la Agano la Mungu.
5Wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. 6Wafilisti waliposikia makelele, wakauliza, “Kwa nini kuna makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?”
Walipofahamu kuwa Sanduku la Mwenyezi Mungu limekuja kambini, 7Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo awali. 8Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. 9Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!”
10Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia kwenye hema lake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari elfu thelathini walioenda kwa miguu. 11Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
Kifo cha Eli
12Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake. 13Alipofika, Eli alikuwa ameketi kwenye kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia.
14Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?”
Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli, 15wakati huu Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane, nayo macho yake yalikuwa yamepofuka hadi hakuweza kuona. 16Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko siku ya leo.”
Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?”
17Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Waisraeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, na wanajeshi wengi sana wameuawa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.”
18Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kwa nyuma kutoka kiti chake kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka arobaini.
19Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mjamzito na alikaribia wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na ya kuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata uchungu naye akajifungua lakini akazidiwa na uchungu. 20Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usiogope, umemzaa mwana wa kiume.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani.
21Alimwita yule mtoto Ikabodi#4:21 maana yake Utukufu umeondoka, akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na mumewe. 22Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.”

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia